19 SEPTEMBA, 2020; JUMAMOSI: JUMA LA 24 LA MWAKA

Mt. Januari, Askofu na Shahidi
Kijani
Zaburi: Juma 4

INJILI: Lk. 8: 1-3
Yesu alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yohana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 56:9-13

 1. Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo.
  Neno hili najua kuwa Mungu yu upande wangu.
  K: Nienende mbele za Mungu katika nuru ya walio hai.
 2. Kwa msaada wa Mungu nitalisifu neno lake.
  Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake.
  Nimemtumaini Mungu, sitaogopa
  Mwanadamu atanitenda nini? (K)
 3. Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu;
  Nitakutolea dhabihu za kushukuru.
  Maana umeniponya nafsi yangu na mauti;
  Je! Hukuizuia miguu yangu isianguke?
  Ili nienende mbele za Mungu
  Katika nuru ya walio hai. (K)

INJILI: Lk. 8:4-15
Mkutano mkuu ulipokutanika, na wale waliotoka kila mji wakimjia, Yesu alisema kwa mfano: Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila. Nyingine zikaanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka kwa kukosa rutuba. Nyingine zikaanguka kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga. Nyingine zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia. Alipokuwa akinena hayo alipaza sauti akisema, Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie. Wanafunzi wake wakamwuliza, Maana yake nini mfano huo? Akasema, Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe. Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu. Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka. Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga. Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote. Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia.

TAFAKARI:
UDONGO MZURI NA MATUNDA YAKE:
Bwana wetu Yesu Kristo leo anatufundisha juu ya mpanzi, mbegu na udongo. Anaweka wazi kwamba ni katika udongo mzuri tu, ndiko mbegu zake ambazo siku zote ni nzuri, matunda mengi huweza kupatikana. Katika ufafanuzi wake, Bwana anasema, “na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno na kulishika, kisha huzaa matunda kwa kuvumilia” (Lk. 8:15). Mbegu hizo ambazo ni Neno la Mungu, linapandwa ndani ya mioyo yetu na Mungu mwenyewe aliye mpandaji, lakini siyo siri kwamba si mara zote hufikia kwa wanaoliamini bali wenye shingo ngumu. Tangu Kristo aanze kutangaza injili yake kwa watu sasa ni miaka karibu 2017, lakini bado Neno halijawaingia watu kwa 100%. Ishara wazi za vita, uonevu, ugandamizaji na uovu unaofanywa na watu mbalimbali ulimwenguni, ni ushahidi wazi kwamba neno la Mungu bado halija pokelewa na watu wengi, vivyo mimi na wewe, tuna kazi ya kulitangaza neno hilo.

SALA: Mwenyezi Mungu, ifungue midomo yangu, nipate kuitangaza Injili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Main Menu